Inawezekana. Powered by Blogger.

TPC Moshi wameonyesha njia, wengine tufuate


Katika harakati za kupambana na tatizo la upungufu wa umeme nchini na kutumia vizuri rasilimali zinazopatikana hapa hapa nchini, Kiwanda cha sukari cha TPC Moshi sasa kinazalisha kiasi cha Megawati ishirini (20MW) kwa kutumia mitambo inayotumia mabaki ya miwa.

Kati ya Megawati ishirini za umeme zinazozalishwa kiwandani hapo, Megawati kumi na moja zinatumika kuendeshea mitambo ya kiwanda hiki na shughuli zote za ofisini kiwandani hapo na pia zinasambazwa kwenye mashamba na vijiji vilivyo jirani na kiwanda hicho. Vijiji vinavyofaidika na umeme huo ni pamoja na Kikavu chini, Mtakuja, Kiyungi na Mvuleni. Megawati tisa zinazosalia zinaingizwa kwenye gridi ya taifa. Kutokana na ubunifu huu, suala la mgawo wa umeme sasa limekuwa ni historia kiwandani hapo.

Ikiwa kiwanda cha sukari TPC Moshi kimeweza, kwa nini wengine tusiweze? Hata kwa kufuata njia hiyo hiyo ambayo TPC Moshi wameipitia, ni kipi kinachotuzuia?

Hapa nchini viko viwanda vingi vinavyozalisha tani nyingi za taka ngumu za namna mbalimbali, kwa nini viwanda hivi na makampuni mengine na watu binafsi tusiwaze namna gani tunavyoweza kuzitumia taka hizo aidha kama chanzo cha nishati au kuzifanya malighafi ya kuzalisha vitu vingine? Tunaweza kufanya mambo haya bila shaka.

Licha ya taka ngumu zinazozalishwa viwandani, lakini pia kuna taka zinazolishwa majumbani, mathalani mabaki ya vyakula na vifungashio vya bidhaa mbalimbali. Taka hizi zinazalishwa kwa wingi sana katika miji yetu kama Dar es Salaam na zinabakia kuwa ni kero kubwa kwa wakazi wa miji hiyo. Taka hizi zinaweza zikatumiwa tena kama malighafi ya kutengeneza nishati  au kutengeza vitu mbalimbali kama mapambo na vinginevyo. Hapo tutakuwa tumefanikiwa kuua ndege wawili kwa jiwe moja. Tutakuwa tunapunguza kero za taka mijini  na pia tutakuwa tunapata malighafi bure na kufanya uzalishaji unaoweza kutuingizia kipato.

Jambo hili linawezekana kabisa. Kinachotakiwa hapa ni ubunifu, kutumia matokeo ya tafiti mbalimbali ambazo zimeshafanywa na kuthubutu.


Post a Comment

About This Blog

  © Blogger template Shush by Ourblogtemplates.com 2009

Back to TOP