Kanuni Muhimu za Kuzuia Magonjwa kwa Ndege Wafugwao
- Jenga mabanda imara ya kuwasetiri ndege dhidi ya upepo na mvua. Hakikisha mabanda haya yana mzunguko wa hewa safi ya kutosha kwa kuweka madirisha makubwa yenye nyavu.
- Waweke ndege wako ndani ya uzio utakaowazuia ndege wako kuchanganyikana na wengine kutoka nje.
- Mabanda ya ndege yafanyiwe usafi mara kwa mara na pia yapuliziwe dawa za kuua wadudu wasumbufu kama viroboto na chawa.
- Wingi wa ndege wako lazima uwiane na ukubwa wa mabanda yako. Sio vizuri ndege wako wakisongamana kwenye eneo moja.
- Wape ndege wako lishe yenye mchanganyiko wa viini lishe vyote muhimu. Ni vizuri maji safi yakawepo wakati wote.
- Tenganisha aina tofauti za ndege, kama kuku, bata, na kadhalika.
- Wape ndege wako chanjo za kuzuia magonjwa mbalimbali.
- Ndege wagonjwa wanapaswa kutengwa na wazima na wapewe uangalizi wa karibu.
- Ndege wanaokufa kwa sababu ya ugonjwa wanapaswa kuchomwa moto au kuzikwa mara moja.
- Wapende ndege wako na uwe karibu nao kila inapowezekana. Hii itakusaidia kutambua kwa urahisi magonjwa au matatizo waliyonayo.